Monday, 5 May 2025

UNAWEZA KUJIAMINI BILA KUONESHA DHARAU?

 

Mchezo wa Masumbwi, ni moja kati ya michezo inayotaka kujiamini pasipo kuonyesha dharau ili kuweza kumshinda mpinzani wako

Kuna mstari mwembamba sana unaotenganisha maana ya neno kujivuna na kujiamini. Ni vigumu sana kumtofautisha mtu anayejivuna au kwa Kiswahili kingine mtu ‘anayejisikia’ na mtu anayejiamini. Lakini hakuna mtu anayependa kufuatana na mtu anayejisikia, hata watu wanajisikia wanakubali kuwa wanachukia majivuno.

Tatizo lililopo katika suala hili ni kwamba watu wengi wanapata tabu sana kutofautisha watu hawa wawili. Mtu anahitaji kujiamini kiasi na siyo kupita kiasi kwa kila jambo. Hivyo mtu anayejiamini ana sifa zipi? Unaweza kumuelezea vipi mtu mwenye majivuno? Na mwisho kabisa, lakini ni muhimu, mtu anaweza je kuwa unajiamini tu bila kujikuta umeingia katika mtego wa watu wenye majivuno? Zijue tofauti hizo:

MTU MWENYE MAJIVUNO
Mtu mwenye majivuno au anayejisikia, siku zote hujiona ndiye bora.
Siku zote hujifanya anajua kitu kilicho bora kwa wengine.
Anapofanya biashara na wengine, hupendi kukopesha.
Daima huwa hakubali makosa yake.
Hufurahi anapoona mwenzake kapatikana makosa.

MTU ANAYEJIAMINI
Mtu huyu hujiamini yeye mwenyewe na kipaji alichonacho.
Huwa muwazi kwa kile anachokusudia kutenda na uwezo alionao wa kufanya kitu.

Hushindana kwa kutumia kipaji alichozaliwa nacho.
Haogopi kukubali makosa yake.
Husaidia wenzie katika kusahihisha makosa yao.

Kujiamini ni tabia ya mtu ambaye anazaliwa nayo. Mtu anayejiamini huwa hajali watu wengine wanamfikiriaje. Hata hivyo mtu mwenye majivuno huwa mwepesi kulalamika anapotendewa vibaya. Hujiona yeye ndiye yeye na tabia hiyo huonesha yeye ni dhalili kiasi gani. Njia pekee anayoweza kuonyesha thamani yake ni kuwadhalilisha watu wanaomzunguka!

JINSI YA KUJIAMINI BILA KUONEKANA UNAJISIKIA

Kuna muongozo wa kufuata ili kuonyesha ni mtu unayejiamini na siyo mwenye majivuno. Kanuni hizi hazina budi kufuatwa muda wote bila kukosa, unapokuwa sehemu zote, kazini na hata nyumbani.

JALI SANA MUONEKANO WAKO (YOUR APPEARANCE)

Katika suala hili, watu wengi hujali vile wanavyotazamwa na watu wengine. Ingawa hapo awali ilielezwa kuwa tabia hii ni ya watu wenye majivuno inaweza kuigwa hata na watu wanaojiamini kwa kiwango fulani, kwa sababu suala la kuvaa na kupendeza ni muhimu kwa wote.

Unapokwenda shughulini, vaa vizuri. Kama wewe ni mfanyakazi na unakwenda kwenye mkutano maalum, basi huna budi kuvaa kiofisa; kama siyo suti nzuri iliyoshonwa na fundi stadi. Uvaaji mzuri, huongeza uwezo wa mtu kujiamini mbele za watu, kwani kama hukuvaa vizuri, huwezi kusimama mbele ya watu kwa kujiamini. Lazima utakuwa na wasiwasi.

TOA TABASAMU LA DHATI

Usitoe tabasamu la uongo, usitabasamu ili watu wakuangalie kuwa una fedha zaidi yao. Toa tabasamu la dhati ili wenzio wakuheshimu na wakuone mtu mwenye furaha na mstaarabu wanaeweza kushirikiana nae katika maongezi na shughuri zingine.

ONYESHA MAPENZI KWA WENZAKO

Kama wewe ni mfanyakazi, unapokutana na wenzako waulize angalau week end zao zilikuwa vipi.

Nia na madhumuni ya kufanya hivyo ni kuwaonyesha kuwa hujioni 'babu kubwa' mbele yao. Kitendo hicho kitawafanya wajisikie na wao ni muhimu na kitaonyesha unawajali. Lakini usifanye hivyo ili kupata nafasi ya kusikilizwa stori zako.

JUA MAMBO MUHIMU YANAYOTOKEA

Penda kusoma magazeti, kusikiliza redio na kuangalia luninga ili kujua nini kinaendelea duniani. Mtu anayejiamini huwa hasiti. Jambo linapojitokeza wakati wa maongezi na wenzako, kuwa tayari kutoa mchango wako wa mawazo. Kuwa na hobi tofauti. Wakati huo huo, kama hujui watu wanaongea nini, ni vizuri kukaa pembeni au kunyamaza.

KUWA MTU MWENYE MSIMAMO

Ni vizuri kuwa na msimamo katika masuala muhimu. Watu wanaojiamini huwa hawaamuliwi au kufanya mambo kwa kushinikizwa. Kuwa na mawazo tofauti katika jambo lile lile.

JUANA NA WATU WENGI
Kujuana na watu wengi humuwezesha mtu kufanya mambo yake kwa kujiamini zaidi. Unaweza kujuana na watu tofauti kwa kujiunga katika vilabu mbalimbali vya burudani, mazoezi au michezo pamoja na kutembelea sehemu mbalimbali.

USIWE MKALI KWA WATU WENGINE
Unaweza kutofautiana na mtu kimawazo bila kuonekana una dharau au majivuno. Kwa mfano, mwenzio au bosi wako anasema jambo ambalo halikukubaliki, eleza kuwa wewe umewahi kufanya makosa kama yake; lakini umeshajifunza kutokana na taarifa mbalimbali ulizokwishapata.

Kimsingi, kila mtu anaweza kujiamini. Elewa kwamba kila mtu hupenda kuwa karibu na mtu anayejiamini na anayefanya mambo yake kwa uhakika. Wapo utakaoweza kweli kujiamini bila shaka mambo mengi yatakunyookea katika shughuli zako za kila siku. Pia kuwa na uhusiano mzuri na watu ni sawa na kumiliki rasilimali yenye thamani kubwa katika maisha.

No comments:

Post a Comment

Licence

Science03

Back To Top